Afisa bandia wa polisi akamatwa Kilimani

Tom Mathinji
1 Min Read
Afisa bandia wa polisi akamatwa.

Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI, wamemkamata afisa bandia wa polisi aanayedaiwa kupokea shilingi milioni 2.5 kwenye sakata ya usajili makurutu wa polisi.

Benedict Odeng’ero Wekesa, alikamatwa baada ya waathiriwa watatu kujitokeza na kuripoti jinsi mshukiwa huyo alivyowahadaa watajiunga na Huduma ya Taifa ya Polisi.

Akiwa na barua bandia za usajili wa makurutu,Wekesa aliwahadaa waathiriwa wake kutoa kiwango kikubwa cha pesa, akiwahakikishia nafasi yao tayari imetengwa.

Kabla ya kugundua walikuwa wakidanganywa, waathiriwa hao walikuwa wametoa kitita cha shilingi milioni 2.5, huku hamu ya kujinunga Huduma ya Taifa ya polisi ikisalia kuwa ndoto.

Maafisa wa polisi walichukua hatua za haraka na kumkamata mshukiwa huyo akiwa amejificha katika hoteli moja eneo la Kilimani Jijini Nairobi, ambapo walipata barua bandia za kujiunga na Huduma ya Taifa ya Polisi.

Hata hivyo mshirika wake alifanikiwa kutoroka kabla ya maafisa hao wa polisi kuwasili.

Kwa sasa Wekesa anazuiliwa kwenye korokoro za polisi, akisubiri kufikishwa mahakamani Jumatatu.

TAGGED:
Share This Article