Abubakar Yakub achaguliwa rais wa AGN

Marion Bosire
2 Min Read

Abubakar Yakubu ndiye rais mpya wa chama cha waigizaji wa Nigeria yaani Actors Guild of Nigeria – AGN kufuatia uchaguzi ulioandaliwa Disemba 6, 2025, na anachukua mahala pa Dr. Emeka Rollas Ejezie.

Yakubu alimshinda Rita Daniels kwenye kinyang’anyiro hicho ambacho kilikuwa na ushindani mkubwa kwenye uchaguzi ulioandaliwa huko Benin jimbo la Edo nchini Nigeria, wakati wa mkutano mkuu wa mwaka.

Yakubu alijizolea kura 116 huku Daniels akizoa kura 113 na kura tatu zikatangazwa kuwa ziliharibika.

Ushindi wa Yakubu ambaye ni mwigizaji na afisa wa usimamizi unachukuliwa kuwa wa kihistoria kwani yeye ndiye rais wa kwanza wa AGN kutoka eneo la Kaskazini mwa Nigeria tangu chama hicho kilipobuniwa mwaka 1998.

Yakubu aliwahi kuhudumu kama katibu wa kitaifa mwaka 2019 hadi 2025 na pia ameshikilia nyadhifa nyingine kama makamu wa rais wa kitaifa, mweka hazina wa kitaifa na afisa wa mahusiano ya umma.

Yeye ni mhitimu wa Sanaa za Maigizo kutoka Chuo Kikuu cha Ahmadu Bello, Zaria na mzaliwa wa Kaduna anayekuja na uzoefu wa zaidi ya miaka 25 katika televisheni, filamu na maigizo ya jukwaani katika wadhifa wake mpya.

Daniels, ambaye ni mama ya mwigizaji maarufu Regina Daniels, alifanya kampeni kwa ajenda ya kulinda na kuwawezesha wanachama.

Hata hivyo, harakati zake zilikumbwa na utata baada ya rais anayeondoka, Rollas, kumshauri hadharani ajikite katika majukumu ya kifamilia.

Katika matokeo mengine, Ifeoma Okeke alichaguliwa kuwa katibu mpya wa kitaifa. Marais wa zamani wa AGN ni pamoja na Larry Williams, Emma Ogugua, Zack Orji, Ejike Asiegbu, Segun Arinze, na Ibinabo Fiberesiman.

Share This Article