Abby Miller aishtaki hospitali ya Cedars-Sinai kwa utepetevu

Mwalimu huyo wa densi anadai fidia kwa kile anachokitaja kuwa kuachiwa kifaa mwilini mwake wakati alifanyiwa upasuaji.

Marion Bosire
1 Min Read

Abby Lee Miller ambaye ni mwalimu wa densi nchini Marekani ameshtaki hospitali moja kubwa ya Los Angeles akidai fidia kutokana na kile anachokitaja kuwa utepetevu wa madaktari.

Miller ameshtaki hospitali ya Cedars-Sinai Marina na madaktari wake wawili akiwalaumu kwa kuacha kifaa kwenye mwili wake walipomfanyia upasuaji wa uti wa mgongo mwaka 2020.

Upasuaji huo ulichukuliwa kuwa uliofanikiwa lakini Abby anasema baadaye alianza kupata maumivu ya tumbo hali ambayo alifahamisha madaktari kadhaa wakiwemo wale wawili waliomhudumia.

Anasema lalama zake zilipuuzwa kwa muda mrefu hadi mmoja wa madaktari wake akaamua kumfanyia uchunguzi wa CT scan ambao ulithibitisha kwamba kuna kifaa kilichokuwa kimeachwa ndani ya mwili wake.

Mcheza densi huyo ambaye amekuwa akiugua ugonjwa wa lymphoma kwa muda na ambaye sasa anatumia kiti cha magurudumu ameshtaki wahusika kwa utepetevu wa kimatibabu, kitaaluma, dhuluma ya kimatibabu kati ya makosa mengine na anataka kulipwa fidia ya dola milioni 1.4.

Msemaji wa hospitali ya Cedars-Sinai alisema hawezi kujadili kwa undani suala ambalo liko mahakamani lakini akatetea taasisi hiyo ya afya akisema huwa inatoa kipaumbele kwa usalama na utunzaji wa wagonjwa, wafanyakazi na wageni.

Share This Article