Rais wa Colombia amjibu Rais Donald Trump

Marion Bosire
2 Min Read

Rais wa Colombia Gustavo Petro amemjibu Rais wa Marekani Donald Trump ambaye alitishia kumchukulia hatua sawia na aliyomchukulia Rais wa Venezuela, Nicholas Maduro.

Trump alikuwa akizungumza na wanahabari Jumapili kwenye ndege yake rasmi ambapo alitishia kwamba atachukua hatua za kijeshi dhidi ya Colombia.

Alisema taifa hilo la Amerika kusini linaugua na linaendeshwa na kiongozi anayeugua anayetengeneza dawa ya kulevya aina ya cocaine ambayo anauzia Marekani.

Petro amekanusha madai hayo ya Trump akisema kwamba yeye ni kiongozi halalai na kamwe hahusiki na biashara ya mihadarati.

“Trump huzungumza bila maarifa. Acha kunisingizia,” aliandika Petro katika chapisho kwenye X.

Kiongozi huyo aliendelea kusema kwamba iwapo Marekani itashambulia Colombia kwa mabomu, hata wakulima wa vijijini watageuka kuwa maelfu ya wapiganaji wa msituni milimani.

Alisema pia kwamba iwapo atazuiliwa huku sehemu kubwa ya nchi ikiwa inampenda na kumheshimu, wataachilia ‘jaguar’ wa watu.

Akiwa kijana, Petro alikuwa mwanachama wa kundi la waasi wa mrengo wa kushoto la M-19, lakini haaminiki kuwahi kushiriki mapigano. Baada kundi hilo kuvunjwa, alishiriki katika kuandaa katiba mpya mwaka 1991 na baadaye akawa mbunge anayeheshimika.

Alikuwa meya wa mji mkuu wa Colombia kabla ya kuchaguliwa kuwa rais.

“Niliapa kutochukua tena silaha … lakini kwa ajili ya taifa nitachukua silaha tena,” alisema.

Waziri wa ulinzi wa Colombia, Pedro Sánchez, alitangaza Jumamosi kwamba ulinzi wa rais umeimarishwa.

Share This Article