Watu wawili wanahofiwa wameaga dunia baada ya jengo la ghorofa 16 lililokuwa likijengwa kuanguka leo Ijumaa katika mtaa wa South C Jijini Nairobi.
Aidha watu kadhaa wanaaminika kukwama kwenye vifusi vya jengo hilo lililoko kwenye barabara ya Muhoho.
Chama cha wakazi wa mtaa wa South C, kimelaani tukio hilo kikiwataka maafisa wote wa serikali ya kaunti ya Nairobi waliohusika na kuidhinisha ujenzi wa jengo hilo kutiwa mbaroni.
“Tunatoa wito kwa serikali ya kaunti ya Nairobi, taasisi za uangalizi na zile za uchunguzi kuchukua hatua za haraka bila mapendeleo,’ alisema mwenyekiti wa chama cha wakazi wa mtaa wa South C Dkt. Abdulmalik Gichuki.
Mbunge wa Lang’ata Felix Odiwour Jalang’o aliyewasili mahala pa tukio, alisema jengo hilo lilikuwa miongoni mwa majengo mengine yaliyosemekana kutokuwa salama.
Jalang’o aliwashutumu maafisa wa kaunti ya Nairobi walioshirikiana na wastawishaji ardhi na kuwaruhusu kujenga bila kufuata kanuni zinazofaa.
Mkurugenzi wa kitengo cha usimamizi wa majanga ya kitaifa Dkt. Duncan Onyango Ochieng alisema watu wengine wawili wanahofiwa kukwama kwenye vifusi vya jengo hilo.
Walioshuhudia na kuzungumza na wanahabari wa runinga ya KBC walisema walinzi wawili walikuwa katika jengo hilo wakati lilipoporomoka.
Juhudi za uokoaji zinaendelea zikiongozwa na wataalamu kutoka kitengo cha kitaifa cha udhibiti wa majanga, vikosi vya jeshi la ulinzi la kenya, huduma ya kitaifa ya polisi pamoja na shirika la msalaba mwekundu.