Vijana Afrika wahimizwa kuongoza kwa ujasiri na uadilifu

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta akiwa Lagos Nigeria.

Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ametambua vijana wa bara Afrika kama rasilimali kubwa zaidi kwenye bara hili huku akiwahimiza kuongoza kwa ujasiri, uadilifu na maono.

Akizungumza Jijini Lagos Nigeria wakati wa tuzo za viongozi wa siku za usoni za mwaka wa 2025, Uhuru alisema mageuzi ya Afrika yataongozwa na raia wake wenyewe, na wala sio suluhu kutoka nje.

“Tumeelezwa kuhusu utajiri mkubwa Barani Afrika, lakini rasilimali yetu kubwa ni fikra na mioyo ya vijana wetu. Nyinyi sio viongozi wa kesho, lakini viongozi wa leo wanaopanga siku za usoni,” alisema uhuru.

Uhuru alitoa changamoto kwa vijana kukumbatia uongozi unaozingatia maadili, uwajibikaji na huduma, akisema Afrika haikosi mawazo wala nguvu, bali inahitaji viongozi wanaozingatia mabadiliko badala ya vyeo.

Aliwapongeza vijana waliotuzwa kwa kuchagua huduma badala ya maslahi ya kibinafsi, akisema juhudi zao zinaonyesha uwezo wa uongozi wa Afrika unaokua.

Kiongozi huyo wa zamani pia alisifia  Mhubiri Chris Oyakhilome kwa kuwalea viongozi vijana kupitia wakfu wa ‘Future Africa Leaders’, akimtambua Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo kwa kuendelea kutoa mwongozo kwa kizazi kijacho cha Afrika.

Share This Article