Rais William Ruto amesema serikali itabuni kitengo cha kukabiliana na ulanguzi wa mihadarati.
Kulingana na kiongozi wa taifa, kitengo hicho kitabuniwa katika Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI, huku kikipewa rasilimali za kisasa, vifaa vya uchunguzi wa kisayansi na uwezo wa kifedha kufanikisha majukumu yake.
“Kitengo hicho kitashirikiana kwa karibu na Halmashauri ya Kitaifa ya kukabiliana na Dawa za kulevya (NACADA), Huduma ya Taifa ya Ujasusi (NIS), Tasisi ya Usimamizi wa Mipaka, Serikali za kaunti na washirika wa kimataifa,” alisema Rais Ruto.
Ili kupiga jeki kitengo hicho, Rais Ruto alisema idadi ya maafisa wake itaongezwa kutoka ile ya sasa ya maafisa 200 hadi maafisa 700, ambao watapokea mafunzo na kupewa vifaa vya kuwawezesha kutekeleza operesheni kote nchini dhidi ya walanguzi, wafadhili na makundi ya wahalifu.
Ili kufanikisha vita dhidi ya ulanguzi wa mihadarati, kiongozi wa taifa alitoa wito kwa idara ya mahakama, kubuni mahakama maalum zitakazoharakisha kesi zinazohusiana na ulanguzi wa mihadarati.
“Nitashauriana na Jaji Mkuu kuhusu jinsi serikali kuu itaisaidia idara ya mahakama ikiwa ni pamoja na utoaji wa rasilimali, huku uhuru wa idara ya mahakama ukiheshimiwa,” aliongeza Rais Ruto
Rais aliyasema Jumatano usiku wakati wa hotuba ya mwaka mpya kwa taifa, katika ikulu ndogo ya Eldoret.