Bunduki 5, risasi 14 zasalimishwa Trans Mara

Tom Mathinji
1 Min Read

Bunduki tano na risasi 14 zimesalimishwa Trans Mara, kaunti ya Narok siku moja baada ya Rais William Ruto kuwaagiza wale wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen,  amewahimiza wale ambao wangali wanamiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha, akisema zaidi ya bunduki 100 zinamilikiwa kinyume cha sheria katika eneo hilo.

“Ili kuwe na amani ya kudumu katika eneo hilo,silaha zote haramu katika maeneo bunge ya  Kilgoris, Kuria East, Kuria West na Emurua Dikirr, sharti zisalimishwe kwa serikali bila kuchelewa. Wale wanaohusika na biashara haramu ya uuzaji wa bunduki na risasi watachukuliwa hatua kali,” alisema Murkomen.

Akizungumza  wakati wa mkutano kuhusu usalama ulioandaliwa Jumanne katika eneo la Siteti, kaunti ndogo ya Trans Mara Kusini, Waziri huyo aliwalaumu baadhi ya walinzi wa misitu katika kaunti hiyo kwa kutumia visivyo bunduki zao.

Waziri huyo alikuwa ameandamana na Naibu Inspekta Mkuu wa Polisi Eliud Lagat, miongoni mwa maafisa wengine wakuu wa usalama.

Share This Article