Mwanamazingira Truphena Muthoni ameteuliwa kuwa balozi wa kampeni ya kitaifa ya upanzi wa miti bilioni 15, inayonuiwa kukabiloiana na mabadiliko ya Tabia Nchi, huku akitunukiwa tuzo ya kutambuliwa na Rais (HSC), baada ya kukumbatia mti wa kiasili kwa saa 72.
Akimkabidhi tuzo hiyo katika Ikulu ya Nairobi, Rais William Ruto alisema Muthoni ametoa hamasisho hapa nchini na kote ulimwenguni kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na Tabia Nchi.
“Katika kutambua ujasiri na uongozi wake wa kupigiwa mfano, nimemteua kuwa balozi wa kampeni ya upanzi wa miti bilioni 15, ambayo inalenga kuhifadhi mazingira hapa nchini,” alisema Rais Ruto.
Wakati huo huo kiongozi wa taifa alisema kuwa wizara ya Mazingira, Mabadiliko ya Tabia Nchi na Misitu, itampiga jeki Muthoni kuafikia ndoto zake kwa kumpeleka nchini Brazil ambako atajifunza mengi kuhusu mbinu za uhifadhi na uongozi wa kimazingira.
Aidha wizara ya Wanyamapori na Bodi ya Utalii zitagharamia likizo ya Muthoni na kundi lake, kama njia ya kutoa shukrani kwa juhudi zake za kuigwa.
Muthoni alivunja rekodi yake ya awali ya kukumbatia mti kwa muda wa saa 48, baada ya kukumbatia mti wa kiasili kwa saa 72.