Ummy Mwalimu azima uvumi ulioenea kumhusu

Marion Bosire
2 Min Read

Ummy Mwalimu ambaye alikuwa mbunge wa eneo la Tanga Mjini, nchini Tanzania na ambaye pia alihudumu kama waziri wa Afya amezima uvumi ambao umekuwa ukienezwa mitandaoni kumhusu.

Mwalimu alichapisha picha ya chapisho la akaunti inayojiita “Tanzania Leaks” ambalo limekuwa likisambaa lenye maneno ya kuashiria kwamba alizuiwa mpakani alipokuwa akisafiri kutoka Tanzania na kuingia Kenya na kwamba yuko mikononi mwa polisi.

Waziri huyo wa zamani aliongeza maneno yake ya kuhimiza umma kupuuza chapisho hilo juu ya picha hiyo na chini yake akaandika,”Nawashukuru wote walionifikia kutaka kujua ukweli kuhusu hii. Ni uzushi. Ipuuzwe. Nipo salama. Alhamdulillah.”

Wanaoendesha akaunti hiyo ya Tanzania Leaks walikuwa wameandika, “Habari za hivi punde: Aliyekuwa mbunge wa Tanga Mjini na waziri wa Afya Ummy Mwalimu yuko kwenye zuio la kusafiri nje ya nchi.”

“Ummy amezuiliwa mpakani Horohoro kuvuka kwenda Mombasa Kenya. Watanganyika na wana CCM kwa ujumla, sio CHADEMA tu, hata CCM tumezuiliwa.” Waliendelea kusema.

Kilichochochea akaunti hiyo kuchapisha habari hizo ambazo kwa sasa zimefutwa hakijulikani lakini ikumbukwe kwamba Tanzania inapitia kipindi kigumu kisiasa baada ya uchaguzi ulioghubikwa na utata.

Ummy hakutetea wadhifa wake kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 na hata kwenye bango alilochapisha mitandaoni la kumpigia debe Rais Samia Suluhu Hassan, alijitambulisha kama mbunge mstaafu wa Tanga Mjini.

Share This Article