Waliohudhuria sherehe za maadhimisho ya siku kuu ya Jamhuri katika uwanja wa Nyayo leo, pamoja na waliokuwa wakifuatilia kupitia runinga walipata burudani tofauti.
Sherehe za kitaifa mara nyingi hupambwa na densi za kitamaduni kutoka jamii mbali mbali na nyimbo za kwaya lakini leo, tume ya kudumu ya muziki ya Rais, PPMC, ilibadili mambo, hazikuwepo.
Burudani ya kawaida ya watoto ambao huvaa sare na kuchora michoro mbali mbali uwanjani wakighani mashairi na kuimba nyimbo zinazoambatana na kauli mbiu nayo haikuwepo.
PPMC iliangazia burudani ya kisasa ikifungua kwa vichekesho kutoka kwa mchekeshaji Captain Otoyo ambaye alizungumzia Ukenya pamoja na utalii ambao ulikuwa kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu.
Tumbuizo lake lilikuwa hata na waigizaji ambao waliigiza kama watalii wa ndani kwa ndani, wakati serikali inahimiza wakenya kuzuru vivutio mbali mbali vya utalii.
Alipomaliza, Otoyo alimwalika mshereheshaji ambaye aliwaalika jukwaani wanamuziki kama Elisha Toto, Dola Kabary, Guardian Angel, Trio Mio na Iyanii.
Wengine waliotumbuiza kwa muziki wao wa kisasa ni kundi la Watendawili lililoimba wimbo wao maarufu wa “Cham Thum”, wakifuatiwa na Sammy Dee aliyeimba wimbo wake “Baba Hoiyee” wa kumkumbuka marehemu Raila Odinga.
Moji Short Baba ambaye huimba nyimbo za kisasa za injili naye alikuwepo jukwaani ambapo alichangamsha waliokuwepo kwa wimbo wake Vimbada.
Wanamuziki wote hao waliambatanisha burudani yao na densi kutoka kwa wacheza densi walioonyesha mitindo ya kisasa ya kusakata densi.