Kiongozi wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka amepongeza mawakili wakuu wapya 54 wapya waliopatiwa hadhi hiyo na Rais William Ruto.
Kalonzo ambaye ni wakili kitaaluma, alisema upanuzi wa ngazi hiyo ya juu ya taaluma ya sheria unaonyesha ukomavu na kina cha taaluma ya sheria nchini Kenya.
Akizungumza jijini Nairobi kwenye hafla ya chajio iliyoandaliwa kwa ajili ya wanachama hao wapya, Kalonzo alisema kuwa kitengo cha mawakili wakuu nchini sasa kina wanachama 120, hatua aliyoitaja kuwa muhimu kwa jamii ya wanasheria.
Alikumbuka na kutoa heshima zake kwa marehemu wakili mkuu Judy Thongori, SC, akimtaja kuwa mtetezi mahiri wa haki za familia na usawa wa kijinsia.
Mwingine aliyemtaja ni marehemu wakili mkuu Mutula Kilonzo na mwenzake Pheroze Nowrojee akiwakumbuka kwa mchango wao katika kuunda mpangilio wa kikatiba wa Kenya.
Kalonzo pia alimtambua Martha Karua, SC, kwa jukumu lake katika uandishi wa Katiba ya 2010.
Makamu huyo wa zamani wa Rais, aliwatambua magwiji wa sheria walio hai, akiwemo aliyekuwa mwanasheria mkuu Amos Wako ambaye pia ni wakili mkuu, Jaji Mkuu mstaafu Willy Mutunga wakili mkuu na aliyekuwa mwanasheria mkuu Githu Muigai wakili mkuu, akiwapongeza kwa uongozi na mwongozo wao kwa taaluma ya sheria.
Kalonzo alisisitiza umuhimu wa kazi ya Paul Ndung’u, ambaye ripoti yake kuhusu ukiukaji wa haki za ardhi aliitaja kuwa ya kihistoria, wakati wakili huyo alipojiunga na kitengo cha mawakili wakuu pamoja na wenzake 53.
Aliwataka mawakili vijana wanaotetea katiba kwa ujasiri waheshimiwe na kusisitiza kuwa utoaji wa hadhi ya wakili mkuu unapaswa kuzingatia uwezo na sifa.
Kalonzo alimalizia kusema kwamba taaluma ya sheria itakuwa na nafasi muhimu katika kulinda uthabiti wa kikatiba wa Kenya kuelekea mwaka 2026 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.