Polisi waliorejea kutoka Haiti watambuliwa kama Mashujaa

Marion Bosire
2 Min Read

Maafisa wa polisi ambao walirejea nchini kutoka Haiti ambako walihudumu kwa miezi 18, leo walipatiwa heshima ya kipekee katika sherehe za kitaifa za siku kuu ya Jamhuri katika uga wa Nyayo, Nairobi.

Mashujaa hao ndio walifunga burudani ya gwaride ya heshima kama ilivyo ada huku wakiwa wamevaa mavazi yao ya kikazi na kubeba bunduki zao.

Kundi hilo ndilo lilikuwa la kwanza kabisa kutumwa katika taifa hilo la Karibea chini ya Kikosi cha Kimataifa cha Usaidizi wa Usalama nchini Haiti.

Walirejea nchini Disemba 9, 2025 na wakaandaliwa hafla ya makaribisho ya kifungua kinywa na Waziri wa usalama wa ndani, Kipchumba Murkomen, katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi wa Utawala kilichopo Embakasi mnamo Desemba 10, 2025.

Wakati wa sherehe za Jamhuri Day za 62, maafisa hao walitunukiwa kwa mafanikio yao katika oparesheni ya Haiti, ambayo iliwezesha miundombinu muhimu nchini humo kurejeshwa kutoka kwa magenge.

Inajumuisha uwanja wa ndege wa kitaifa, shule na vituo vya afya pamoja na maeneo mengine muhimu ambayo maafisa walikomboa kutoka kwa magenge.

Maafisa watatu waliopoteza maisha yao katika operesheni ya kukabiliana na magenge ya Haiti pia walikumbukwa kama mashujaa.

Katika sherehe za Jamhuri maafisa hao walishangiliwa na umati uliofurika katika uwanja wa Nyayo, walitanguliwa na maafisa wa GSU na kufuatwa kwa karibu na maafisa wa doria mpakani.

Gwaride ya maafisa hao waliotoka Haiti ilikuwa na bendera tatu ambazo ni bendera ya kijani ya polisi, bendera ya Huduma ya taifa ya Polisi na bendera ya Polisi wa Utawala.

Walipatiwa heshima kamili ya waliokuwepo uwanjani Nyayo akiwemo Rais William Ruto ya kusimamiwa kwa muda mfupi huku nao walipiga saluti walipofika mbele ya jukwaa kuu.

Share This Article