Rais William Ruto ametoa wito wa kutekelezwa haraka kwa maazimio ambayo bado hayajatekelezwa kutoka kwa mikutano ya awali ya kati ya serikali za kitaifa na kaunti, akionya kuwa ucheleweshaji unaweza kudhoofisha mafanikio ya ugatuzi nchini.
Alikuwa akizungumza katika mkutano wa 12 uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi ambapo alisifia ushirikiano imara kati ya serikali kuu na serikali za kaunti, akisema umeimarisha ugatuzi na kuboresha utoaji huduma kote nchini.
Ruto alibainisha kuwa kaunti zimepiga hatua kubwa katika kuimarisha huduma za afya kupitia mageuzi ya mamlaka ya afya ya jamii, kukuza mifumo ya thamani ya kilimo, kuendeleza maeneo ya kuongeza thamani ya bidhaa, Viwanda na kuweka mifumo ya kidijitali ili kuongeza ufanisi.
Kiongozi wa nchi alisisitiza pia kuhusu ushirikiano na washirika wa kimataifa kama Marekani, katika kuimarisha mifumo ya afya inayosimamiwa kwa pamoja na ngazi zote mbili za serikali.
Rais aliongeza kuwa kukamilika kwa kihistoria kwa ugatuzi, uainishaji na kuchapishwa rasmi kwa majukumu ya kaunti ni hatua muhimu inayotoa uwazi wa majukumu na kuhakikisha rasilimali zinafuata majukumu hayo.
Akitambua maendeleo yaliyopatikana hadi sasa, Ruto alizitaka taasisi zinazosimamia utekelezaji wa maazimio ya awali ya Mkutano huo kuchukua hatua kwa haraka.
Ruto alisisitiza kuwa utekelezaji kamili ni muhimu katika kudumisha mfumo wa ugatuzi unaozingatia wananchi na unaojibu mahitaji ya watu.