Rais wa chama cha wanamuziki nchini Uganda UMA, Cindrella Sanyu maarufu kama Cindy amewapa changamoto wanamuziki wa kike wanaokua kwa kasi nchini humo Ava Peace na Jowy Landa, akitaka washindane jukwaani.
Cindy ambaye amekuwa akiimba kwa muda na ambaye anachukuliwa kuwa mtumbuizaji bora anahisi kwamba shindano kama hilo litawafaidi wasanii, mashabiki na tasnia nzima ya muziki.
“Ninafikiri wasichana hawa wawili wanafaa kushindana jukwaani, hiyo ndiyo njia pekee ya kufahamu ni nani malkia halisi” alisema Cindy akiongeza kwamba malkia atajitosa jukwaani na kudhihirisha uwezo wake.
Alikiri kwamba hajamwona Jowy kwenye majukwaa makubwa lakini ana talanta na kusisitiza wanafaa kushindana na katika harakati hizo wajipatie mapato.
Cindy alisema pia kwamba Ava Peace ni mmoja wa wasanii chipukizi ambao wana vipaji vya kipekee ba wabastahili kuwa malkia wa muziki wa Uganda.
Uimbaji wa Ava Peace ni wa kuvutia ambapo wengi wamekuwa wakimfananisha na Sheebah Karungi kwa jinsi anatumbuiza vizuri jukwaani, mavazi, maumbile na hata rangi ya ngozi.
Jowy Landa kwa upande wake anakua kwa haraka katika tasnia ya muziki ambapo amejitengenezea nafasi yake kwa mtindo wa afrobeats na muziki wa kisasa.
Pendekezo hilo la Cindy Sanyu linajiri siku chache tu baada yake kukataa kushindana jukwaani na Sheebah Karungi kwa mara nyingine.
Alikuwa akihojiwa ambapo alisema mwaka 2023, alimshinda Sheebah na kufanya shindano jingine naye itakuwa sio haki.