Kenya yawapeleka maafisa wa polisi 230 nchini Haiti

Tom Mathinji
1 Min Read
Kenya yawapeleka maafisa 230 wa polisi kukabiliana na magenge ya wahalifu nchini Haiti.

Kenya imetuma kikosi cha maafisa 230 wa Huduma ya Taifa ya Polisi nchini Haiti, kuungana na vikosi vinavyokabiliana na magenge ya wahalifu nchini humo (GSF).

Akizungumza alipokuwa akiliaga kikosi hicho, mshauri wa maswala ya usalama katika afisi ya Rais, Balozi Dkt. Monica Juma, alisema kuwa maafisa hao wanatoka kwenye vitengo mbalimbali vya huduma ya kitaifa ya polisi, na watajiunga na maafisa wa usalama kutoka nchi nyingine zinazoshiriki, ikiwa ni pamoja na Jamaica, Guatemala, El Salvador, Bahamas, na Belize.

Huku akiwasilisha ujumbe wa heri njema kutoka kwa Rais William Ruto, Juma aliwahimiza maafisa hao kuwa mabalozi wema na alipongeza mafanikio makubwa yaliyoafikiwa tayari nchini Haiti.

Alisema kuwa doria zinazofanywa kwa ushirikiano kati ya maafisa wa usalama waliopelekwa nchini humo na wale wa Haiti zimeongeza utulivu na kufanikisha kukamatwa kwa wahalifu katika maeneo yanayodhibitiwa na magenge yakiwemo jiji la Port-au-Prince, Ganthier, na Delmas.

Dkt. Juma alikuwa ameandamana na maafisa wakuu wa Huduma ya Taifa ya Polisi.

Share This Article