Wananchi watakiwa kusalia nyumbani kesho nchini Tanzania

Marion Bosire
2 Min Read
Mwigulu Nchemba, Waziri Mkuu wa Tanzania

Wananchi wa Tanzania wameagizwa kusalia nyumbani kesho Disemba 9, 2025, ambayo ni siku kuu ya uhuru ya Tanzania bara, ambayo pia ni siku ambayo maandamano yamepangiwa kufanyika nchini humo.

Waziri mkuu wa taifa hilo Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ndiye alitoa tahadhari hiyo alipokuwa akiwasilisha ujumbe wa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu siku kuu ya kesho.

Katika ujumbe huo Rais Samia aliwatakia raia wote kheri ya siku kuu hiyo ambayo huadhimishwa kila mwaka.

“Ndugu wananchi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anapenda kuwatakiwa wananchi wote heri ya siku kuu ya uhuru wa Tanania bara.” alianza Nchemba.

Kiongozi huyo aliongeza kusema kwamba wananchi wote ambao hawatakuwa na dharura wanafaa kusalia nyumbani na kutumia siku hiyo kwa mapumziko huku wale ambao kazi zao zinawahitaji sana wakitakiwa kuwa kwenye vituo vyao vya kazi.

Ujumbe huo unaashiria kwamba hakutaandaliwa sherehe za kitaifa za maadhimisho ya siku kuu hiyo kama ilivyo ada, hatua inayoamikika kulenga kuzuia maandamano yaliyopangwa.

Ijumaa polisi wa Tanzania nao walitoa onyo kuhusu maandamano hayo wakiyataja kuwa kinyume cha sheria.

Wahusika wa maandalizi ya maandamano hayo walisema ni ya kulalamikia vifo vilivyotokea baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 nchini humo ambapo Rais Samia aliibuka mshindi katika kinyang’anyiro cha urais.

Share This Article