Washukiwa wanne wa ulaghai unaohusu zabuni ya huduma katika idara ya Magereza walitiwa mbaroni na maafisa wa upelelezi wa jinai wa huko Kitui ya kati.
Clement Wachira, Andrew Kimani, Ann Waweru na Rehema Makandi, walibuni mpango wa ulaghai ambapo walijisingizia kuwa maafisa wa ngazi za juu katika idara ya magereza na kumtapeli mfanyabiashara mmoja shilingi elfu 105.
Mfanyabiashara huyo alikuwa ameahidiwa kwamba atapatiwa zabuni ya kuvutia ya kupeleka mboga katika gereza kuu la serikali la Kitui na wakati aligundua haikuwa ahadi ya ukweli tayari alikuwa ameporwa pesa hizo.
Maafisa wa upelelezi waliokuwa wakifuatilia kisa hicho kwa wiki kadhaa walifumania washukiwa hao wakiwa ndani ya gari aina ya Toyota Harrier ya rangi nyeusi nambari ya usajili KCV 543W inayoaminika kutumika katika utapeli wao.
Msako wa maafisa wa upelelezi kwenye gari hilo ulinasa fomu gushi 37 za kuidhinisha zabuni, vitambulisho gushi viwili vya kazi katika idara ya magereza, simu 8 za mkononi na vitambulisho 6 vya kitaifa.
Wanashikiliwa na maafisa wa polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani.
Maafisa wa upelelezi nao wanaendeleza uchunguzi kubaini iwapo kuna wahasiriwa wengine wa kundi hilo la matapeli kando na mfanyabiashara huyo.