Mzozo wazuka upya kati ya Pakistan na Afghanistan

Tom Mathinji
1 Min Read
Mapigano yazuka upya kati ya Pakistan na Afghanistan.

Mzozo umezuka upya kati ya Pakistan na Afghanistan katika mpaka karibu na mji wa Spin Boldak, huku pande zote mbili zikilaumiana kwa kukiuka mkataba wa kusitisha vita.

Kulingana na taarifa, Hospitali ya Kandahar imepokea miili ya watu wanne, huku Pakistan ikiripoti majeruhi watatu.

Msemaji wa Waziri Mkuu wa Pakistan alisema Taliban ilianza mashambulizi “bila sababu”, na kwamba jeshi la nchi hiyo lilijibu mapigo “vikali”. Taliban nayo ilidai Pakistan “imeanzisha mashambulizi tena”, hivyo wakaamua kujitetea.

Video zinaonyesha raia wengi wakikimbia kwa miguu na kwa magari kutokana na hofu ya mapigano kuongezeka.

Mapigano haya yametokea chini ya miezi miwili tangu Qatar na Uturuki kusaidia kufikia usitishaji mapigano uliomaliza vita vikali zaidi kati ya pande hizo tangu 2021.

Hata hivyo, uhasama bado uko juu. Pakistan imekuwa ikiituhumu Taliban kuwahifadhi wapiganaji wanaoishambulia, madai ambayo Taliban inakanusha na kusema Pakistan inalaumu watu wengine kwa “kushindwa kwake katika eneo la usalama”.

Wiki iliyopita, duru ya nne ya mazungumzo ilifanyika Saudi Arabia, lakini hakuna makubaliano mapya yaliyofikiwa. Hata hivyo, vyanzo vinaeleza kuwa pande zote mbili zilikubaliana kuendelea kuheshimu usitishaji mapigano.

Share This Article