Washukiwa watatu wakamatwa kwa madai ya wizi wa ardhi ya NSSF

Tom Mathinji
1 Min Read
Washukiwa watatu wakamatwa kwa madai ya ulaghai wa ardhi.

Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), wamewakamata wanaume watatu wanaodaiwa kuhusika katika ulaghai mkubwa wa ardhi.

Kulingana na idara hiyo, ulaghai huo unahusisha mali inayomilkiwa na hazina ya kitaifa ya Malipo ya Uzeeni NSSF, yenye thamani ya shilingi milioni 350.

Watatu hao Harish Ramji, Ashvin Ramji na Bharat Ramji, walikamatwa baada ya wapelelezi hao kuwahusisha na ununuzi wa kipande cha ardhi cha hekta 3.043 eneo la Athi River kaunti ya Machakos.

DCI imesema kesi hiyo ilianzishwa kufuatia lalama zilizowasilishwa mapema mwezi Septemba, wakati NSSF iliripoti kwamba watatu hao walikuwa wamepata hatimiliki ya kipande hicho cha ardhi na kudai kuuziwa na hazina hiyo.

Baada ya uchunguzi, wapepelezi hao walibaini kuwa mnamo mwezi Mei mwaka 2010, washukiwa wakisaidiwa na washirika wao ambao wangali kukamatwa walighushi nyaraka ya mauzo ya ardhi hiyo ikiwa na sahihi za wadhamini wa bodi ya NSSF.

Viongozi wa mashtaka walikagua nyaraka hizo na kukubaliana na wapepelezi hao na kuidhinisha mashtaka ikiwa ni pamoja na njama ya kulaghai, utengenezaji nyaraka bandia, na kupata usajili kwa njia ya uongo na ulaghai.

Watatu hao kwa sasa wanazuiliwa wakisubiri kushtakiwa. Juhudi za kuwakamata washukiwa wengine zingali zinaendele.

TAGGED:
Share This Article