Kenya yaridhia pendekezo la kuendeleza AGOA

Marion Bosire
2 Min Read

Kenya imeridhia pendekezo la serikali ya Marekani la kuongeza muda wa mkataba wa AGOA kwa mwaka mmoja.

Rais William Ruto alisema hatua hiyo itasaidia kudumisha uthabiti wa biashara huku mataifa hayo mawili yakifanya kazi ya kuunda mfumo wa kina wa muda mrefu.

Alitoa kauli hiyo baada ya kufanya mazungumzo na mwakilishi wa kibiashara wa Marekani, Balozi Jamieson Greer, mjini Washington, D.C.

Rais Ruto alisema mazungumzo hayo yalilenga kuanzisha makubaliano mapya ya kibiashara baina ya nchi hizo mbili ili kuimarisha ushirikiano kati ya Nairobi na Washington.

Alibainisha kuwa Kenya na Marekani zinaunda mfumo wa pamoja utakaoboresha mazingira ya uwekezaji na kufungua fursa zaidi za kibiashara kwa pande zote mbili.

Kwa mujibu wa Rais, pande hizo mbili zimembaini sekta muhimu za upanuzi, zikiwemo mavazi na nguo, bidhaa za kilimo, ngozi na viatu, kemikali na dawa, pamoja na teknolojia ya habari na huduma za kidijitali.

Sekta hizi alisema zina uwezo mkubwa wa kuongeza ajira, mapato ya kuuza nje na kuimarisha minyororo ya thamani nchini.

Ruto alikaribisha pendekezo la Marekani la kuongeza muda wa AGOA—ambalo kwa sasa linasubiri idhini ya Congress—akibainisha kuwa Balozi Greer alisema kuongeza muda huo kutatoa nafasi kwa serikali kuandaa mpango thabiti na mpana zaidi unaonufaisha maslahi ya kiuchumi ya pande zote.

AGOA, iliyoanzishwa mwaka 2000, inatoa upendeleo wa kuuza bidhaa zaidi ya 1,800 bila ushuru katika soko la Marekani kwa nchi zinazostahili za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Lengo lake ni kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia upatikanaji mpana wa masoko, utawala bora na kukuza misingi ya soko huru.

Share This Article