Uncle Chumi aitisha pesa alizomtunuku Sheebah jukwaani

Marion Bosire
1 Min Read

Uncle Chumi ambaye ni msanii wa muziki na mchekeshaji tata nchini Uganda, amezua gumzo mitandaoni baada ya kudai arejeshewe pesa alizomzawadi mwanamuziki mwenza Sheebah wakati wa tumbuizo la moja kwa moja jukwaani.

Chumi ambaye jina lake halisi ni Mushabe Crek Haidare, alikuwa mubashara kwenye TikTok, ambapo aliwakosoa Sheebah na Ritah Dancehall, akisisitiza kwamba wawili hao wanapaswa kurejesha shilingi milioni 3 alizowapa jukwaani.

Kulingana naye, wakati akitoa pesa hizo alikuwa amelewa kidogo na sasa anataka arejeshewe ili azitumie kwa mambo mengine.

“Sheebah Malkia, miaka yote ambayo mmekuwa mkitumbuiza jukwaani na Ritah Dancehall, hamjui kutofautisha mtu aliyelewa kidogo na aliye sawa? Niliwapa pesa zangu milioni 3 nanyi mkaziweka mfukoni.” alisema Chumi.

Aliendelea kusema kwamba anataka pesa zake zirudi akiongeza, “Tafuteni namna ya kuzikusanya na mrejeshe.”

Tukio hili linaongezeka kwenye orodha ndefu ya matukio ya sarakasi yanayomhusu Uncle Chumi, ambaye amejijengea sifa ya utata mtandaoni na nje ya mtandao.

Mashabiki wengi watakumbuka ugomvi wake mkali na Spice Diana, uliotokana na kutokuelewana kuhusu remix waliyoifanyia pamoja.

Mzozo huo hatimaye uliua kabisa uhusiano wao.

Hadi sasa, Sheebah na Ritah Dancehall hawajatoa majibu ya wazi kuhusu madai ya kurejesha pesa. Mashabiki wanasubiri kwa hamu kuona jinsi wanamuziki hao wawili watakavyoshughulikia tuhuma hizo.

Share This Article