Serikali imeuza asilimia 15 ya hisa za Safaricom kwa kampuni ya Vodacom katika mkataba wa biashara kwa thamani ya shilingi bilioni 240.5.
Hii ni sehemu ya mpango wa kufungua uwekezaji wa kibinafsi bila kuinua viwango vya kodi au deni la taifa. Baada ya uuzaji huo, serikali itadumisha asilimia 20 ya hisa katika kampuni ya Safaricom.
Waziri wa fedha John Mbadi amesema mkataba huo unapiga jeki ajenda ya serikali ya kuvutia uwekezaji katika mali muhimu pamoja na miundomsingi.
Shughuli hiyo ya biashara inategemea idhini kutoka kwa wadhibiti nchini Kenya, Ethiopia na Afrika Kusini. Safaricom itasalia kwenye orodha ya soko la Hisa la Nairobi.
Afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Vodacom Shameel Joosub alisema hatua hiyo ni muhimu katika mkakati wa kampuni hiyo wa kupanua masoko yake barani Afrika pamoja na kuimarisha huduma za kifedha na kidijitali nchini Kenya na Ethiopia.
Baada ya ununuzi, Vodacom inapanga kununua asilimia 5 ya hisa kutoka Vodafone kwa shilingi 34, kwa kila hisa na kuongeza jumla ya hisa zake za Safaricom kutoka asilimia 35 hadi 55.