Mwaura aonya wanaokejeli walemavu kwa misingi ya mwonekano

Marion Bosire
2 Min Read

Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura, ametoa onyo kali kwa watu wanaowakejeli au kuwadhihaki walemavu kwa misingi ya mwonekano wa miili yao, akisema kuwa hatua zitachukuliwa dhidi ya wanaokiuka sheria na haki za watu wenye ulemavu.

Akizungumza katika afisi za chama cha wasio na uwezo wa kuona jijini Nairobi jana katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya walemavu, Mwaura alisema kuwa ubaguzi na dhihaka vinavyotokana na ulemavu havina nafasi katika jamii yenye haki.

Alitoa taarifa yake ya kila wiki kwa wanahabari katika hafla hiyo yenye kaulimbiu “Kujenga Jamii Jumuishi kwa Watu Wenye Ulemavu Ili Kuendeleza Maendeleo ya Kijamii”.

Mwaura alieleza mafanikio ya serikali kupitia Ajenda ya Mageuzi ya Kiuchumi ya Chini kwenda Juu (BETA) na Mkataba wa Uchumi kwa Watu Wenye Ulemavu, akisisitiza kuwa ujumuishaji wa watu wenye ulemavu ni ajenda kuu ya kitaifa.

Ajenda hiyo kulingana naye imekitwa katika Katiba, Sheria ya Watu Wenye Ulemavu na Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu Wenye Ulemavu.

Alibainisha juhudi zinazoendelea za kupanua ulinzi wa kijamii kupitia ruzuku za fedha, kuboresha upatikanaji wa ufadhili kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati kwa watu wenye ulemavu, kuboresha huduma za afya kupitia vifaa saidizi na kuimarisha elimu jumuishi.

Mwaura pia alisisitiza dhamira ya serikali ya kuhakikisha mawasiliano yanafikiwa na wote, ikiwa ni pamoja na matumizi ya lugha ya ishara na kampeni za uhamasishaji kuhusu haki za watu wenye ulemavu.

Alithibitisha kwamba serikali itaendelea kuhimiza jamii inayowaheshimu, kuwalinda na kuwajumuisha ipasavyo watu wenye ulemavu katika maendeleo ya taifa.

Share This Article