Jaji Mkuu Martha Koome amehimiza kuimarishwa kwa mbinu za utoaji wa haki za familia zinazozingatia misingi ya kijamii, akitaka mageuzi.
Mageuzi hayo kulingana naye yanafaa kutambua hali halisi ya familia za Kenya zinazokumbwa na changamoto za ndoa za kimila ambazo hazijasajiliwa chini ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 2014.
Aliyasema hayo katika Kongamano la Kwanza la ‘Inns of Court’ la Kitengo cha familia cha milimani lililofanyika jijini Nairobi.
Katika hotuba yake kuu yenye mada “Sheria ya Ndoa 2014: Athari za Ndoa za Kimila Zisizosajiliwa katika Migogoro ya Familia” Jaji Mkuu alisifu Kitengo cha Familia cha Milimani, Majaji, na Kamati ya Mawakili na Majaji kwa kuanzisha jukwaa bunifu la majadiliano ya kisheria.
Alikitaka Chuo cha idara ya mahakama kuiga mfano huo katika vitengo vingine vya mahakama kuu.
Akirejelea safari ya Kenya katika utoaji haki za familia, Jaji Mkuu alibainisha kuwa migogoro ya familia awali ilishughulikiwa kama kesi za kiraia za kawaida, mara nyingi mbele ya maafisa wa mahakama wasio na ujuzi.
Ujuzi huo ni kuhusu kushughulikia changamoto za kisaikolojia na kijamii zinazohusiana na malezi, ukatili wa majumbani na masuala ya ndoa.
Kuanzishwa kwa Kitengo cha Familia mwaka 2000, alisema kulileta mabadiliko muhimu kuelekea kwenye mkondo wa hukumu unaolenga kuponya na kulinda watu walio hatarini.
Jaji Mkuu Koome alitaja mafanikio chini ya mkakati wa Mabadiliko ya Kijamii Kupitia Upatikanaji wa Haki, yakiwemo kuanzishwa kwa Mahakama ya Kwanza Maalum ya Familia katika ngazi ya Hakimu mwaka 2023.
Mahakama hiyo imeongeza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma na ufanisi, ikishughulikia takriban kesi elfu 6, mwaka 2024 pekee na kukamilisha zaidi ya 3,000 kati yazo.