Trump kukutanisha Kagame na Tshisekedi leo

Marion Bosire
2 Min Read
Rais wa Marekani Donald Trump.

Rais wa Marekani Donald Trump hii leo, Disemba 4, 2025 anatarajiwa kuwakutanisha viongozi wa nchi za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ikulu ya White House ilikuwa imetangaza awali kwamba Rais Trump ametoa mwaliko kwa Marais Paul Kagame na Felix Tshisekedi ambapo wanatarajiwa kutia saini mkataba wa amani na ushirikiano kiuchumi.

Wadadisi wanahisi kwamba kiongozi huyo wa Marekani atapata tena sababu ya kujigamba kwa kufanikisha mapatano kwa mara nyingine na kusistisha vita.

Hatua hii inafuatia hatua ya mawaziri wa masuala ya nchi za kigeni wa mataifa hayo mawili ya Afrika kutia saini mkataba wa awali wa amani na ushirikiano wa kiuchumi katika ikulu ya Marekani mwezi Juni.

Mazungumzo ya miezi kadhaa yalifuatiwa na mkutano huko Qatar mwezi Novemba ambapo walitia saini mfumo unaolenga kukomesha mapigano ya miaka kadhaa.

Waasi wa M23 wamekuwa wakipigana na wanajeshi wa serikali ya DRC katika mkoa wa Kivu Kaskazini kwa muda wa zaidi ya miaka 10, mzozo ulioota kutoka kwa mauaji ya halaiki ya mwaka 1994.

Kundi hilo la waasi ambalo lilikuwa likififia liliibuka tena mwaka 2021 ripoti zikiashiria kwamba zamu hiyo lilikuwa likiungwa mkono na serikali ya Rwanda.

Rwanda imekuwa ikikanusha madai hayo ikisema kwamba wanajeshi wake mara kwa mara wamelazimika kujilinda kutokana na mashambulizi ya wanajeshi wa DRC na wapiganaji wa kabila la Hutu mpakani.

Watu wengi wameuawa kwenye mapigano hayo yaliyopamba moto mwanzo wa mwaka huu ambapo M23 ilichukua udhibiti wa majiji makubwa ya DRC.

Mapigano yamekuwa yakiendelea sambamba na mchakato wa kutafuta amani huku wengi wakitilia shaka iwapo mkataba unaotarajiwa kutiwa saini leo utasitisha makabiliano kabisa.

Share This Article