Wafanyabiashara wa mbao watakiwa kuchangia upanzi wa miti

Marion Bosire
2 Min Read
Dkt. Deborah Barasa - Waziri wa Mazingira

Wahusika wa biashara ya mbao nchini wametakiwa kuchangia katika kampeni endelevu ya upanzi wa miche bilioni 15 inayoendeshwa na serikali.

Wito huu ulitolewa na waziri wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi na misitu Deborah Barasa, wakati wa mkutano wa mashauriano huko Arboretum Nairobi.

Waziri huyo alisema kuwa kampeni ya upanzi wa miti bilioni 15 itahakikisha uendelevu wa sekta hiyo, akibainisha kuwa sekta hiyo hupata malighafi moja kwa moja kutoka misitu ya umma.

Alihimiza wamiliki wa viwanda vya kukata mbao kuunga mkono lengo la kuongeza utandu wa misitu nchini hadi asilimia 30 kupitia urejeshaji wa maeneo yaliyoharibika.

Barasa aliomba wawekezaji kufikiria kushiriki mpango huo kwa kuchukua maeneo maalum ya misitu, kusaidia shule kupanda miti, na kurejesha ikolojia katika maeneo ya mikoko kwenye ukanda wa pwani miongoni mwa mengine.

Juhudi hizi zote, alibainisha, zitachangia katika urejeshaji wa mandhari ya taifa.

Waziri huyo pia alibainisha kuwa mchakato wa ukataji wa miti iliyokomaa na iliyozidi umri unaendelea kwa uwazi, na kwamba uadilifu katika mgao utafuatwa kulingana na kanuni za Serikali.

Mwenyekiti wa Bodi ya Huduma ya Misitu Kenya -KFS, Titus Korir, alieleza kuwa wawekezaji katika sekta ya mbao ni wadau muhimu wanaosaidia kuzalisha sehemu kubwa ya mapato ya Huduma hiyo.

Mkuu wa uhifadhi wa misitu Alex Lemarkoko naye alishauri wenye viwanda vya mbao kuanzisha vitalu vya miti ili kuhakikisha uendelevu wa juhudi zao za upandaji miti.

Share This Article