Murkomen: Magenge ya wahalifu ni tisho kwa usalama wa taifa

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, amesema kuwa wahuni na magenge ya wahalifu ni tisho kwa usalama wa taifa na kwamba Inspekta Mkuu wa Polisi anaendelea kuweka mikakati ya kuyaangamiza,

Kulingana na waziri huyo, wanasiasa hutumia magenge hayo kwa manufaa yao ya kisiasa.

“Katika sehemu zingine, magenge hayo hugeuza hafla za mazishi kuwa ghasia na kuwawekea mzigo mkubwa machifu manaibu wao na maafisa wanaosimamia vituo vya polisi,” alisema Murkomen.

Baadhi ya magenge ambayo waziri huyo aliyataja ni pamoja na Watizedi, Confirm, Gaza, 42 Brothers, Panga Boys, MRC, Mungiki, Sungu Sungu na Chinkororo.

Murkomen aliongeza kuwa serikali imejitolea kikamilifu kukabiliana na wanaovunja sheria, wakiwa kwa serikali au upinzani kudumisha amani na kulinda taifa.

Akizungumza leo Jumanne wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Jukwaa la Usalama katika Ikulu ya Nairobi, waziri huyo pia alidokeza kuwa ujangili na ugaidi bado ni changamoto kubwa ya kiusalama humu nchini, hasa katika maeneo ya kaskazini na yale ya mipakani.

Murkomen alisema kuwa ujangili, unaojumuisha wizi wa mifugo na mashambulizi, ni tatizo la muda mrefu katika eneo la kaskazini, lililochangiwa na umaskini, ushindani wa rasilimali, na miundombinu duni. Hata hivyo, Murkomen alisema serikali imepiga hatua kubwa kukomesha uhalifu huo.

“Ujangili unaendelea kuwa changamoto katika baadhi ya sehemu za hapa nchini, lakini hatua kubwa zimechukuliwa hasaa katika maeneo kama bonde la kerio ambapo amani inashuhudiwa,” alisema Murkomen.

Wakati huo huo kwenye ripoti hiyo, waziri  alisema dhuluma za kingono na kijinsia ni tatizo kubwa hapa nchini, akiongeza kuwa baadhi ya visa hivyo huwahusisha wale ambao wanaposwa kuwalinda watoto.

“Tunataka kuimarisha vita dhidi ya dhuluma hizi,” alisema Murkomen.

Ripoti hiyo iliandaliwa baada ya Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, kuandaa mikutano ya Jukwaa la Usalama katika kaunti zote, kupokea maoni ya kiusalama kutoka kwa wadau wote wa usalama hapa nchini.

Share This Article