Wafanyakazi watatu wa wizara ya Leba wakamatwa kwa kushiriki ufisadi

Tom Mathinji
1 Min Read
Wafanyakazi watatu wakamatwa kwa kushiriki ufisadi.

Maafisa wa Tume ya Maadili na kukabiliana na Ufisadi (EACC), wamewakamata maafisa watatu wa wizara ya Leba katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), kwa madai ya kuwaitisha hongo mawakala wanaofanikisha usafiri wa wafanyakazi wanaoelekea katika mataifa ya mashariki ya kati.

Watatu hao walikamatwa baada ya Tume hiyo kupokea habari iliyodai kuwa maafisa wa wizara ya Leba katika uwanja wa JKIA hudai na kupokea hongo mara kwa mara kwa kila mfanyakazi anayesafiri kwenda mataifa ya mashariki ya kati.

Kupitia kwa taarifa kwenye ukurasa wa X, EACC ilisema kuwa maafisa wake walifanya uchunguzi na kuthibitisha kuwa, mawakala hao walikuwa wakilipa shilingi 500 kwa kila mfanyakazi kabla ya wafanyikazi hao kuruhusiwa kusafiri.

“Mnamo Novemba 30,2025, tume hii ilitekeleza operesheni kwa ushirikiano na wakala mmoja aliyekuwa na wafanyakazi 78 waliokuwa wakielekea Mashariki ya Kati. Wakala huyo alikutana na wafanyakazi hao watatu wa wizara ya Leba, ambapo maafisa hao waliitisha hongo ya shilingi 34,000,” ilisema EACC kwenye ukurasa wa X.

Washukiwa hao watatu walipelekwa katika makao makuu ya EACC, kuandikisha taarifa.

Share This Article