Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni hatahudhuria mjadala wa wawaniaji Urais, haya ni kulingana na chama chake cha National Resistance Movement – NRM.
Runinga ya NTV imeandaa mjadala wa wanaowania Urais nchini humo utakaoandaliwa Jumapili na kupeperushwa moja kwa moja kwenye runinga hiyo.
Majadala huo unajiri miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa Januari 2026 na uamuzi wa Museveni unaachia wapinzani wake jukwaa la kujadiliana na umma.
Katika taarifa iliyochapishwa jana usiku, NRM ilikanusha rasmi madai kwamba Rais angehudhuria mdahalo huo, uliopangwa kufanyika saa 2 usiku Jumapili, tarehe 30 Novemba 2025.
Chama hicho kilitaja sababu za kiutawala na ratiba kuwa misingi ya uamuzi huo.
“Tumeona tangazo linalosambaa kwenye mitandao ya kijamii kutoka kwa NTV Uganda, likidai kuandaa mdahalo wa Urais… Kwa rekodi, NRM ilipokea mwaliko tarehe 21 Novemba 2025, muda mrefu baada ya tume ya uchaguzi kuridhia ratiba za kampeni za wagombea” taarifa ya NRM ilisomeka.
Chama hicho kiliendelea kusema kwamba mdahalo huo haukuwasilishwa kwa wagombea mapema na hivyo haukujumuishwa kwenye ratiba iliyoidhinishwa na Tume ya Uchaguzi.
“Mgombea wetu wa Urais kwa hiyo haandaliwi kushiriki mdahalo wowote wa aina hiyo” iliendelea kusema taarifa ya NRM.
Wagombea wengine kama Robert Kyagulanyi Ssentamu maarufu kama Bobi Wine wamethibitisha kushiriki mdahalo huo.