Huku chaguzi ndogo zikitarajiwa kuandaliwa kote nchini siku ya Alhamisi, wakazi wa eneo bunge la Mbeere Kaskazini, kaunti ya Embu wamehimizwa kujitokeza kupiga kura ili kutekeleza haki zao za kikatiba.
Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku amesema serikali imeweka mikakati yote ya kiusalama kuhakikisha zoezi hilo linatekelezwa kwa amani.
Akizungumza na wanahabari mjini Embu leo Jumatano, waziri alielezea matumaini kwamba mgombea kiti cha eneo hilo wa chama cha UDA Leonard Wamuthende ataibuka mshindi.
” Tuna matumaini kwamba Leo Wamuthende ataibuka mshindi,” alisema Ruku.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Gavana wa Embu Cecily Mbarire, aliwashukuru wakazi wa Mbeere Kaskazini kwa kudumisha amani wakati wa kipindi cha kampeni.
Gavana huyo aliyepia mwenyekiti wa chama cha UDA, aliwahimiza wakazi wa eneo bunge la Mbeere Kaskazini kupiga kura kwa amani wakati wa uchaguzi huo mdogo.
”Tunawashukuru watu wote wa Mbeere North kwa kudumisha amani wakati wa kapeni na tunawahimiza wajitokeze kupiga kura,” alisema Mbarire.
Kiti cha eneo bunge la Mbeere Kaskazini kilisalia wazi baada ya aliyekuwa mbunge wa eneo Geoffrey Ruku kuteuliwa na RAIS William Ruto kuwa Waziri wa Utumishi wa Umma.