Mfanyabiashara wa Tanzania Jennifer Jovin maarufu kama Niffer, ambaye alikamatwa na baadaye kushtakiwa kwa kosa la uhaini, alirejeshwa rumande jana huku washtakiwa wenzake wakiachiliwa.
Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa ameagiza kufutiliwa mbali kwa kesi zote za uhaini dhidi ya waliokamatwa kuhusiana na vurugu zilizoshuhudiwa wakati wa uchaguzi nchini humo.
Kutokana na hilo, mkurugenzi wa mashtaka ya umma – DPP nchini Tanzania jana aliondoa mashtaka na kuwaachilia huru washtakiwa 20 kati ya 22 waliokuwa wakituhumiwa kwa makosa ya uhaini.
Licha ya uamuzi huo washtakiwa wawili, ambao ni Niffer wa umri wa miaka 26 na Mika Lucas Chavala ambaye ni msimamizi wa Swahili Nation Network walirejeshwa rumande.
Hatua hiyo ilitangazwa jana Novemba 25, 2025, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Aaron Lyamuya, kufuatia maelezo ya Wakili wa Serikali Titus Aron, ambaye aliieleza mahakama kuwa DPP hatarajii kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa 20 waliotajwa katika kesi hiyo.
Niffer alikuwa amekamatwa kabla ya uchaguzi akidaiwa kuchochea na kuhamasisha watu kuzua vurugu wakati wa uchaguzi mkuu mwisho wa mwezi Oktoba.
Mama yake mzazi ambaye alikuwa amefika mahakamani kwa matumaini kwamba ataungana tena na binti yake aliangua kilio nje ya mahakama baada ya kufahamu kuwa yeye sio mmoja wa walioachiliwa huru.
Inasubiriwa kuona jinsi kesi yake itaendeshwa huku wanamitandao wengi nchini Tanzania wakimwombea Niffer kwamba naye apate uhuru wake anedelee na maisha yake.