Rais William Ruto amesema kwamba Afrika iko tayari kushirikiana na washirika wanaoleta thamani katika ardhi ya Afrika kwa kujenga viwanda ili kuunda fursa kwa vijana.
Kiongozi wa nchi alibainisha kuwa bara hili lazima libadili kutoka ushirikiano wa unyonyaji hadi ule wa uzalishaji, kutoka kusafirisha malighafi hadi kusafirisha ubunifu na bidhaa zilizokamilika.
Rais Ruto alisema hayo, alipohutubia mkutano wa 7 wa Umoja wa Afrika – AU na Umoja wa Ulaya – EU uliofanyika Luanda, Angola.
Alisema ili kuongeza ushirikiano na washirika kama Umoja wa Ulaya, Afrika inaongeza ujumuishaji wa kibiashara, kwa jumuiya za kiuchumi za kikanda kama msingi na Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA), soko moja la watu bilioni 1.4, kama injini kuu.
Aliitaka EU kuungana na Afrika katika kusukuma mbele mabadiliko ya kidijitali ili kufungua fursa mpya, kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kuunga mkono uhamaji wa wafanyakazi kwa njia ya haki na iliyoratibiwa.
Kiongozi wa nchi pia aliongoza kikao cha kamati maalum ya marekebisho ya kitaasisi katika Umoja wa Afrika ambapo alisema marekebisho ya Umoja wa Afrika ni hatua ya dharura na muhimu.
Mabadiliko hayo anasema yatahakikisha kwamba umoja wa Afrika unaendeleza sauti na ajenda ya Afrika kwa ufanisi.
“Bila mabadiliko ya maana, AU iko katika hatari ya kupoteza ufanisi, jambo ambalo litatugharimu zaidi kwa kupoteza fursa na kupungua kwa ushawishi.” Alisema Rais Ruto.
Kulingana na kiongozi wa nchi, ripoti aliyowasilisha kwenye mkutano huo inagusia maeneo manane ya kipaumbele ambayo ni kufufua muundo wa amani na usalama, ufadhili, kuanzisha Mahakama ya Haki ya Afrika na kurahisisha mpangilio wa ajenda ya AU.
Mengine ambayo viongozi walijadiliana kwenye kikao hicho ni pamoja na kuboresha upya bunge la Afrika, kupanga maamuzi katika makundi, kugawa majukumu na mabadiliko ya kinadharia ya vyombo, taasisi na afisi zilizobaki za AU.
Rais Ruto anahisi kwamba marekebisho haya yanawezekana akisema, “Tushirikiane ili kufanya ndoto hii itimie”.