Shughuli za Upanuzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Naivasha hadi Kampala, Rwanda hadi katika mpaka wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, zitaanza mapema mwaka ujao.
Rais William Ruto amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha biashara na utangamano wa watu kati ya nchi hizo mbili na Jamii ya Afrika Mashariki kwa jumla.
Kiongozi wa taifa aliyasema hayo Jumapili alipokuwa katika eneo la Osukuru, wilaya ya Tororo , nchini Uganda, alipoungana na Rais Yoweri Museveni wakati wa hafla ya ufunguzi wa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha vyuma cha Devki.
”Mnamo mwezi Januari, tutazindua upanuzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Naivasha hadi Kampala na baadaye hadi DRC,” alisema Rais Ruto.
Wakati huo huo, Rais Ruto alisema mataifa hayo mawili pia yatashirikiana kwa pamoja katika shughuli za upanuzi wa bomba la mafuta hadi Rwanda na DRC, kama sehemu ya juhudi za kuimarisha uhusiano wa kikanda na ushindani wa kiuchumi.
Kenya inauza asilimia 64 ya umiliki wake katika kampuni ya Kenya Pipeline kupitia soko la hisa.
Hata hivyo rais Ruto alibainisha kuwa miradi ya kikanda kama vile mabomba ya mafuta, reli ya SGR, na uunganishi wa barabara ya Rironi–Nakuru–Eldoret–Malaba zimeundwa ili kuimarisha uunganishaji kati ya pwani na bara, na kuunda mapito mapya ya kiuchumi.