Maafisa wa shirika la kukabiliana na matumizi ya pombe na mihadarati NACADA waliongoza oparesheni iliyonasa pombe bandia ya thamani ya shilingi milioni 14 huko Kitui.
Oparesheni hiyo ya usiku iligundua shehena kubwa ya pombe ya kiwango cha pili iliyokuwa imefichwa katika bohari moja viungani mwa mji wa Kitui.
Pombe hiyo ilijumuisha chupa elfu 57 za pombe aina ya spirits na kemikali mbali mbali zinazotumika kutengeneza mvinyo huo.
Huo ulikuwa mwendelezo wa msako ulioanza Jumanne na kusababisha kuharibiwa kwa kiwanda haramu cha kutayarisha pombe katika eneo la Wikililye huku mshukiwa mmoja akikamatwa.
Kulingana na maafisa, wahusika wa kiwanda hicho huenda wakawa kwenye kundi moja kubwa la kugushi pombe huku wakifichua kiwango kikubwa cha faida inayotokana na biashara hiyo haramu.
Afisa mkuu mtendaji wa NACADA Antony Omerikwa, ametoa onyo kali kwa wanaoendeleza biashara hiyo haramu kwa bidhaa hizo zinazodhuru afya ya wanaotumia.
“Shehena hii ya thamani ya milioni 14 sio takwimu tu bali ni shehena na miili mitarajiwa imekamatwa. Hatuwezi kutulia tu watu kama hawa wakifaidi kwa kuharibu jamii” alisema Omerikwa.
Mkurugenzi huyo wa NACADA alisisitiza kujitolea kwa serikali kukaniliana na biashara hiyo haramu akiapa kumsaka kila mhusika na kuhakikisha anachukuliwa hatua za kisheria.
Wakazi wa Kitui walishangazwa na upatikanaji wa shehena hiyo ya pombe haramu na washukiwa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kitui Central wakisubiri uchunguzi ukamilike.