Tamasha maarufu la Uganda Nyege Nyege kuanza kesho

Marion Bosire
2 Min Read

Awamu ya mwaka huu ya tamasha maarufu la Uganda Nyege Nyege inaanza kesho hadi Novemba 24, 2025, katika eneo la maanguko ya maji la Kalagala katika wilaya ya Kayunga.

Kaulimbiu ya awamu hiyo ya 10 ya tamasha la nyege nyege ni “Ekiggunda Ky’omuliro” yaani “Mkutano wa Miale ya Moto” na watakaohudhuria watafurahia burudani ya kipekee.

Kulingana na waandalizi, wasanii watakaotumbuiza ni zaidi ya 300 kwenye hatua sita tofauti, zikichanganya muziki wa kielektroniki wa majaribio, Afro-house, midundo ya kitamaduni na tamaduni za muziki wa kilabu kutoka kote duniani.

Msanii mashuhuri wa kimataifa Skrillex kutoka Marekani ni miongoni mwa vivutio vikubwa zaidi na itakuwa mara yake ya kwanza kabisa kutumbuiza kwenye tamasha la nyege nyege.

Wasanii wengine waliothibitishwa kuhudhuria na kutumbuiza ni pamoja na Flowdan wa Uingereza, DJ Travella wa Tanzania na Boutross wa Kenya, miongoni mwa wengine wengi.

Kando na muziki kutakuwa na jukwaa la filamu, maonyesho ya mitindo yaitwayo ‘Kwetu Kwanza’ na kongamano jipya la muziki wa kielektroniki wa Afrika.

Wapenzi wa michezo ya majini pia wana sababu ya kufurahi kwani eneo hilo la maanguko ya maji la Kalagala linatoa fursa ya kucheza michezo hiyo.

Awamu ya mwaka 2024 ya tamasha la nyege nyege iliandaliwa katika uwanja wa mchezo wa gofu wa Jinja na chanzo cha mto Nile huko huko Jinja nchini Uganda

Share This Article