Trump aipa Wizara ya Sheria siku 30 kuachia faili za Epstein

Marion Bosire
2 Min Read

Rais wa Marekani Donald Trump ameagiza Wizara ya Sheria ya nchi hiyo kuachia faili zote zinazohusiana na uchunguzi wa marehemu Jeffrey Epstein katika muda wa siku 30.

Kiongozi huyo alitangaza jana Jumatano kwamba amesaini mswada unaoagiza kuachiwa kwa faili zote za Epstein, aliyekuwa amehukumiwa kwa makosa ya unyanyasaji wa kingono.

Mswada huo unahitaji wizara hiyo kuachia taarifa zote kutoka katika uchunguzi wake dhidi ya Epstein zikiwa katika mfumo unaoweza kutafutwa na kupakuliwa mtandaoni ndani ya siku 30.

Awali, Trump alipinga kuachiwa kwa faili hizo, lakini alibadilisha msimamo wiki iliyopita baada ya kukabiliwa na upinzani kutoka kwa waathiriwa wa Epstein na wanachama wa Chama chake cha Republican.

Sheria hiyo aliyotia saini, ilipitishwa kwa wingi katika mabaraza yote mawili ya Bunge, Baraza la Wawakilishi na Seneti, siku ya Jumanne.

Wabunge katika Baraza la Wawakilishi walipitisha sheria hiyo kwa kura 427-1 huku Seneti ikitoa ridhaa kwa kauli moja kuipitisha mara ilipowasili na kupeleka mswada kwa Trump ili autie saini.

Katika chapisho kwenye Truth Social jana Jumatano, rais aliwatuhumu Democratic kwa kulikuza suala hilo ili kupotosha umakini kutoka kwa mafanikio ya utawala wake.

Faili za Epstein zinazopaswa kuachiliwa chini ya sheria hiyo ni nyaraka kutoka uchunguzi wa jinai kuhusu mfadhili huyo, pamoja na nakala za mahojiano na waathiriwa na mashahidi, na vitu vilivyokamatwa wakati wa uvamizi wa makazi zake.

Vifaa hivyo vinajumuisha mawasiliano ya ndani ya wizara ya sheria, rekodi za safari za ndege na watu au taasisi zilizounganishwa na Epstein.

Faili hizo ni tofauti na zaidi ya kurasa 20,000 za nyaraka kutoka kwa nyumba ya Epstein zilizotolewa na Congress wiki iliyopita, ikiwa ni pamoja na baadhi zinazomtaja Trump moja kwa moja.

Trump alikuwa rafiki wa Epstein kwa miaka mingi, lakini amesema walitofautiana mapema miaka ya 2000, miaka miwili kabla Epstein hakukamatwa kwa mara ya kwanza. Amekana mara kwa mara kufanya kosa lolote kuhusiana na Epstein.

Share This Article