Waziri wa madini, uvuvi na uchumi samawati, Ali Hassan Joho, amewataka wakazi wa Magarini kulichukulia kwa umakini unaostahili uchaguzi mdogo ujao kwani utatoa mwelekeo wa siasa za baadaye za eneo zima la Pwani.
Akizungumza katika eneo la Sabaki baada ya mikutano ya kampeni katika maeneo ya Marafa na Chamara, Joho alisema kumchagua Harrison Kombe kutaimarisha nafasi ya kisiasa ya eneo hilo ndani ya chama cha ODM na pia katika mpangilio mpana wa kisiasa.
“Uchaguzi huu mdogo si kuhusu Harrison Kombe pekee bali mustakabali wetu kama watu wa Pwani. Katika kambi ile nyingine hatuna mwakilishi, lakini katika ule mpangilio mpana tunao Joho, Amason Kingi, Salim Mvurya, Gideon Mung’aro, Abdulswamad Nassir, Seneta Stewarts Madzayo, maseneta wengine kadhaa pamoja na wabunge na madiwani. Ushindi wa Kombe ni ushindi wetu sote kwa sababu utatupa sauti ya kisiasa katika ngazi ya kitaifa,” alisema.
Waziri Joho alikuwa ameandamana na Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro, Wabunge Amina Mnyazi wa Malindi, Paul Katana wa Kaloleni na Mishi Mboko wa Likoni, pamoja na wawakilishi wa kike Getrude Mbeyu wa Kilifi na wenzao wa Kwale na Mombasa Fatuma Masito na Zamzam Mohamed.
Kampeni za chaguzi ndogo zinazopangiwa kuandaliwa katika maeneo mbali mbali nchini Novemna 29, 2025 zinaendelea kushika kasi huku kila chama na mrengo kikijaribu kujipima nguvu kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.