Benki ya Dunia imeunga mkono mpango kabambe wa Kenya wa kuanzisha hazina ya kitaifa wa miundombinu, hatua inayolenga kuharakisha maendeleo makubwa katika sekta za uchukuzi, unyunyiziaji mashamba maji na uzalishaji wa nishati kote nchini.
Kulingana na Benki hiyo, pendekezo la Kenya kujenga mabwawa makubwa 50 kwa lengo la kuongeza eneo la kilimo cha unyunyiziaji mashamba maji kwa ekari milioni 2.5 linawakilisha njia mwafaka zaidi kwa nchi kufanikisha uzalishaji wa chakula endelevu na ulioboreshwa.
Kutokana na ukweli kwamba asilimia 85 ya eneo la Kenya ni kame na nusu-kame, Benki hiyo ilibainisha kuwa kilimo cha unyunyiziaji mashamba maji kimegeuka kuwa nguzo muhimu ya kuongeza usalama wa chakula, kwani kilimo cha kutegemea mvua kwenye asilimia 15 tu ya ardhi inayolimika kimefikia kikomo.
Hazina ya kitaifa ya miundombinu inatarajiwa kuhamasisha rasilimali kwa ajenda pana ya maendeleo, mipango ikihusisha ujenzi wa mabwawa 50 na ujenzi wa kilomita 20,000 za barabara mpya.
Mingine ni pamoja na upanuzi wa njia kuu kwa kuzifanya kuwa za safu mbili umbali wa kilomita 2,000 na uzalishaji wa megawati 10,000 zaidi za umeme ili kuimarisha sekta ya utengenezaji na viwanda.
Kando na miundombinu ya kifizikia, Benki ya Dunia imethibitisha upya msaada wake kwa vipaumbele vya Kenya katika maendeleo ya kijamii.
Hivi ni pamoja na kuimarisha mifumo ya elimu, utoaji wa huduma za afya, programu za ulinzi wa kijamii na maendeleo ya rasilimali watu.
Maendeleo haya yalijadiliwa katika kikao kilichofanyika Ikulu, Nairobi, kati ya uongozi wa Kenya na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia kwa Afrika, kutoka Africa Group One, Zarau Kibwe.
Viongozi wa Kenya walishukuru Benki hiyo kwa ushirikiano endelevu katika ajenda ya maendeleo ya kitaifa na uwekezaji katika sekta za kijamii.
Serikali inasema hazina hiyo mpya itakuwa na nafasi muhimu katika kufungua ukuaji wa muda mrefu, kupunguza tofauti za kimaeneo na kuiweka Kenya kama kitovu cha kiuchumi katika ukanda huu.