Rais William Ruto amehimiza majaji wawe wakitanguliza haki, ujasiri na uhuru wanaposhughulikia kesi za wakimbizi na wahamiaji.
Alikuwa akizungumza alipokuwa akifungua rasmi awamu ya 14 ya kongamano la ulimwengu la muungano wa majaji kuhusu wakimbizi na uhamiaji hapa Nairobi.
Kongamano hilo linaandaliwa kuanzia leo Novemba 17 hadi 19, 2025 na litafuatiwa na warsha za kuimarisha utaalamu Novemba 20 hadi 22, 2025.
Katika hotuba yake Rais Ruto alidhihirisha kujitolea kwa taifa hili katika jukumu la kuhifadhi wakimbizi akisema Kenya ndiyo hifadhi kubwa zaidi ya wakimbizi ulimwenguni ikiwa na wakimbizi laki 8.
“Ili kuhakikisha wakimbizi wanajenga upya maisha yao kwa njia ya hadhi, tunaimarisha mifumo yetu ya kisheria na kitaasisi kupitia mipango kama Shirika Plan” alisema kiongozi wa nchi.
Rais alisema kwa jitihada hizo, Kenya inatambua kikomo cha uwezo wake, na akaisihi jumuiya ya kimataifa kugawana wajibu kwa usawa zaidi kupitia msaada wa kifedha, uwekaji upya wakimbizi, na ushirikiano wa kiufundi.
Alisisitiza kwamba mshikamano wa kweli sio hisani, bali ni kujitolea kwa ajili ya haki kwa wakimbizi wakati suluhu za kudumu na endelevu zinazorejesha amani na utulivu katika nchi zao za nyumbani zinatafutwa.
Rais alimalizia kwa kusema kwamba kudumisha kwa uadilifu, ujasiri na uhuru katika kesi hizo kutahakikisha kwamba kila mkimbizi na mhamiaji anasikilizwa na kutendewa kwa heshima na utu.