Mwenyekiti wa mamlaka ya kudhibiti bidhaa bandia, ACA, Josphat Gichunge Kabeabea amefunguliwa mashtaka na afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma ODPP.
Kabeabea analaumiwa kwa kuitisha na kupokea hongo ya shilingi milioni 5 kutoka kwa mfanyabiashara, na alifikishwa mbele ya mahakama ya kupambana na ufisadi ya Milimani.
Upande wa mashtaka, ukiongozwa na Wesley Nyamache, ulimweleza Hakimu Mkuu Mwandamizi Celesa Okore kwamba mwenyekiti huyo wa bodi ya ACA alitafuta kujinufaisha kinyume cha sheria kwa kutoka kwa mfanyabiashara Du Zhisheng.
Inadaiwa kuwa rushwa hiyo ilitakiwa kama malipo ili kumpa mhusika upendeleo katika kesi inayohusiana na vipuri vya magari vinavyoshukiwa kuwa bandia.
Upande wa mashtaka uliiambia mahakama kwamba kosa hilo lilitokea tarehe 11 Novemba 2025 na DPP alikubali mashtaka hayo baada ya kudurusu ushahidi uliokusanywa na wapelelezi.
Kabeabea alikana mashtaka hayo na akaachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni 2 au milioni 1 pesa taslimu.
Kama sehemu ya masharti ya dhamana, mahakama iliamuru Josphat Gichunge Kabeabea akabidhi pasi yake ya usafiri.
Alizuiwa pia kuwasiliana au kuingilia mashahidi wa upande wa mashtaka ili kuhakikisha uadilifu wa kesi hiyo inapoendelea.
Kesi hiyo itatajwa tarehe 8 Disemba mwaka huu wa 2025, ambapo mahakama itatoa maelekezo zaidi.