Mwanamuziki wa Uganda Geoffrey Kyagambiddwa, maarufu kama Chagga Yagga amekanusha madai kwamba alipokea usaidizi wa kifedha kutoka kwa Eddy Kenzo na shirikisho la wanamuziki UNMF kwa ajili ya tamasha lake.
Tamasha hilo lililofaa kuandaliwa mapema mwezi huu, lilifutiliwa mbali baada ya mwandaaji kukosa kulipa wengi wa watoa huduma na kusababisha mgogoro.
Baada ya kufutwa kwa tamasha hilo, taarifa zilienea kwamba Chagga alipokea pesa kutoka kwa Kenzo na Shirikisho la UNMF, jambo lililochochea ukosoaji mtandaoni.
Hata hivyo, Chagga ametokea wazi na kukanusha madai hayo vikali. Alifafanua kwamba Kenzo alikuwa ameahidi kuunga mkono tamasha hilo kwa kutumbuiza tu, na si kwa kutoa fedha.
“Sijawahi kupokea kiasi chochote cha pesa kutoka kwa Kenzo kama ufadhili wa tamasha langu. Msaada wake ulikuwa ni kuonekana kimwili kwenye onyesho, sio pesa.” alielezea.
Aliendelea kusema kwamba Kenzo aliahidi kumuunga mkono kwenye tamasha, na kweli alitoka mashambani hadi mjini kwa ajili ya tukio hilo hata kama halikufanyika.
Chagga alionyesha masikitiko na kukata tamaa akisema anahisi kusalitiwa na marafiki waliomwangusha katika kile kilichokuwa hatua muhimu sana katika taaluma yake.
Anasema ametumikia na kupambana pamoja na wengi kwenye tasnia kwa miaka mingi, lakini walishindwa kujitokeza wakati alipowahitaji zaidi.