Serikali imesema itahakikisha chaguzi ndogo za mwezi Novemba zinaandaliwa katika mazingira salama na ya amani.
Hayo yalisemwa na waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen wakati wa ibada ya Jumapili katika Kanisa la St. Luke Methodist, Kariene Kaunti ya Meru.
Murkomen alisema wizara yake haitaruhusu visa vya ukosefu wa usalama katika maeneo ambayo chaguzi ndogo zitaandaliwa tarehe 27 mwezi huu.
Aidha waziri huyo aliwapongeza wakazi wa eneo hilo kwa kudumisha amani kupitia operesheni ya Maliza Uhalifu iliyofanikisha kukabiliana na wizi wa mifugo katika eneo hilo.
“Tunaimarisha operesheni kuhakikisha amani ya kudumu pamoja na kubuni afisi zaidi za serikali kuhakikisha huduma za serikali zainakuja karibu na wananchi,” alisema Murkomen.
Kuhusu usajili wa makurutu, Murkomen alisema zoezi hilo ni sehemu ya juhudi za serikali za kuimarisha usalama wa taifa kwa kuajiri wafanyakazi wenye ujuzi chini ya mfumo wa usawa.
Kadhalika, alisisitiza kwamba mchakato wa ajira utafuatiliwa kwa karibu ili kuhakikisha uwazi, haki na fursa sawa kwa wote waliohitimu.