Azawi aelezea kuhusu kutohusika kwenye kampeni

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa kike nchini Uganda Azawi ameelezea sababu ya kutotaka kuhusika kwenye kampeni zinazoendelea za uchaguzi mkuu wa mwaka ujao nchini humo.

Azawi ambaye jina lake halisi ni Priscilla Zawedde alikuwa akihojiwa ambapo alisema kwamba aliamua kutounga mkono upande wowote kisiasa kwani hataki kuwa kibaraka wa serikali.

Msajiliwa huyo wa kampuni ya Swangz Avenue tangu mwaka 2019, amejitenga na wasanii wengi ambao wanahudhuria mikutano ya kampeni na hata kutumbuiza.

Usemi wa Azawi unajiri wakati ambapo nchi hiyo ya Afrika mashariki inajiandaa kwa uchaguzi wa mwezi Januari mwakani na wasanii wakionyesha wazi kwamba wanamuunga mkono Rais Yoweri Museveni na chama chake National Resistance Movement- NRM.

Wasanii ambao wameonekana wakifanya hivyo ni pamoja na Ronald Mayinja, Jose Chameleone, Alien Skin, Catherine Kisasira, Lil Pazo, Weasel Manizo na wengine.

Bebe Cool na Eddy Kenzo, ambaye ni Rais wa shirikisho la wanamuziki wa Uganda UNMF na mshauri wa Rais kuhusu wabunifu ndio wanashirikisha uhusika wa wanamuziki kwenye kampeni hizo za NRM.

Share This Article