Kamati ya uwekezaji wa umma kuhusu utawala na elimu, inayoongozwa na Wanami Wamboka mbunge wa Bumula imeibua wasiwasi kuhusu matumizi ya fedha na utawala wa vyuo.
Jana kamati hiyo iliandaa kikao cha kuchunguza mienendo ya utawala na usimamizi wa fedha katika taasisi za elimu ya juu na za kiufundi.
Wakati wa asubuhi, chuo kikuu cha Koitaleel Samoei kiliangaziwa ambapo ripoti za ukaguzi zilionyesha kuwa vifaa vya thamani ya shilingi 1,307,059 vilitolewa bila maagizo rasmi au idhini ya wakuu wa idara.
Uongozi wa chuo ulielezea kwamba mapungufu hayo yalitokana na changamoto za wafanyakazi wakati wa kuanzishwa kwa chuo hicho chini ya aliyekuwa Mkuu wa Chuo, Prof. Gideon Misoi.
Kamati hiyo hata hivyo ilisisitiza kuhusu uwajibikaji na kudai udhibiti mkali zaidi.
Wabunge walibaini kukosekana kwa nyaraka muhimu kama hati za usafirishaji, ankara na ripoti za ukaguzi kuhusiana na jenereta ya dharura na ujenzi wa tanki la maji lililoinuliwa, miradi iliyogharimu jumla ya shilingi 10,234,176.
Taasisi hiyo iliagizwa kuwasilisha nyaraka hizo ndani ya wiki moja, pamoja na maelezo kamili ya wafanyakazi waliokuwa wakijihusisha na kazi za ujenzi, kufuatia dalili kuwa baadhi ya wafanyakazi walilipwa ada iliyo chini kwa kiwango cha asilimia 30 ikilinganishwa na viwango vya soko.
Wajumbe wa baraza la zamani waliwekewa deni la shilingi 764,600 kwa malipo yasiyo halali ya usafiri na malazi, fedha ambazo lazima zirudishwe ndani ya miezi mitatu.
Kikao cha mchana cha kamati hiyo jana, kiliangazia Baraza la Chuo Kikuu cha Maasai Mara ambalo liliitwa kufika mbele ya kamati tarehe 3 Desemba 2025 baada ya kukosa kufika mara sita.
Wabunge wanatarajiwa kukagua miradi ya chuo hicho na kuchunguza kumbukumbu zake. Kamati ilihoji uamuzi wa kurekebisha basi chakavu kuwa mkahawa wa wafanyakazi ilhali timu ya kiufundi ilikuwa imependekeza liondolewe kabisa.
Wajumbe pia walipinga malipo ya safari na vikao ya jumla ya shilingi milioni 13.2 kwa wajumbe wa baraza waliokuwa wameomba udhuru; nyaraka za mahudhurio ya chuo zilipingwa na uhakiki zaidi ukaamriwa.
Wahusika watakatwa pesa hizho kutoka kwenye mishahara yao.
Chuo kikuu cha Maasai Mara kilibainika pia kutumia huduma za kisheria za thamani ya shilingi milioni 12 bila kufuata taratibu za ununuzi zilizokubaliwa.
Kakai Bisau mwanachama wa kamati hiyo ya bunge kuhusu uwekezaji wa umma katika elimu na utawala, alilitaja hatua hiyo kuwa ya kutia wasiwasi unaoweza kusababisha matumizi mabaya ya fedha za umma.
Mwenyekiti Wamboka alisisitiza kuwa usimamizi wa bunge upo hai na hautakuwa na upole, akisema, “Kamati hii itafanya ukaguzi wa maeneo, itafuatilia nyaraka ambazo bado hazijawasilishwa, na itahakikisha urejeshaji wa fedha na adhabu kwa wale waliotumia vibaya rasilimali za umma, ili kulinda fedha za walipa kodi na kurejesha imani ya umma.”