Msomi wa masuala ya sheria wa asili ya Kenya Profesa Phoebe Okowa ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ, ambayo ni taasisi ya Umoja wa Mataifa.
Okowa aliibuka mshindi baada ya awamu nne za upigaji kura katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA na katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, UNSC.
UNSC ilisema katika taarifa kwamba Okowa alichaguliwa na wengi na anajiunga na majaji wengine 14 wa mahakama hiyo.
Majaji wa ICJ huwa wanahudumu kwa muhula wa miaka 9 huku uchaguzi wa nyadhifa tano kati ya zote 15, ukiandaliwa kila baada ya miaka mitatu kama njia ya kuhakikisha uendelevu.
Rais wa UNSC Michael Imran Kanu alimfahamisha Okowa kuhusu kuteuliwa kwake kupitia barua rasmi.
“Nina furaha kukufahamisha kwamba katika mkutano wa 10040 wa Baraza la Usalama ulioandaliwa Novemba 12, 2025 kwa ajili ya kuteua Jaji kujaza wadhifa ulioachwa wazi Septemba 30, 2025, uliteuliwa kujaza wadhifa huo,” alisema Kanu katika batua hiyo.
Okowa amekuwa raia wa kwanza wa Kenya aliyezaliwa Kenya kuwahi kushikilia wadhifa huo na wa tano kutoka bara Afrika.
Jaji Abdulqawi Ahmed Yusuf mzaliwa wa Somalia aliyechukua uraia wa Kenya alihudumu katika mahakama hiyo baada ya kuteuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2009 na mara ya pili mwaka 2018.
Yusuf alihudumu pia kama Rais wa mahakama hiyo mwaka 2018 hadi 2021 na hivyo kuwa Mwafrika wa kwanza kuwahi kushikilia wadhifa huo tangu mwaka 1994.