Mke na mwana wa Ali Bongo miaka 20 jela

Marion Bosire
2 Min Read
Ali na Sylvia Bongo Ondimba

Mke wa aliyekuwa Rais wa Gabon Ali Bongo na mwanao wa kiume wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani kila mmoja baada ya kesi ya ufsadi dhidi yao iliyofanyika kwa siku mbili.

Hukumu hiyo ilitolewa jana Jumanne Novemba 12, 2025 na mahakama moja ya Gabon dhidi ya Sylvia Bongo na Noureddin Bongo ambao walipatikana na hatia ya matumizi mabaya ya fedha za umma na ufisadi.

Wawili hao ambao hawakuwepo mahakamani pia walitozwa faini ya dola 177,000, huku Noureddin akiagizwa kulipa Dola milioni 2.1 zaidi kutokana na madhila aliyosababishia nchi ya Gabon.

Walilaumiwa kwa kutumia vibaya hali ya Ali Bongo baada yake kukumbwa na kiharusi mwaka 2018 kuipora Gabon kujitosheleza kibinafsi.

Walikana madai dhidi yao hata kabla ya kesi hiyo kuanza wakiitaja kuwa sarakasi ya kisheria.

Ali Bongo aliondolewa madarakani Agosti 2023 katika mapinduzi yaliyoongozwa na Brice Oligui Nguema,ambaye sasa ameacha uanajeshi na alichaguliwa Rais wa nchi hiyo mwanzo wa mwaka huu.

Baada ya serikali ya Bongo kupinduliwa, mkewe na mwanao walikamatwa nchini Gabon wakakaa kizuizini kwa miezi 20 kabla ya kuachiliwa huru mwezi Mei na kuruhusiwa kwenda London kwa matibabu.

Rais wa zamani Ali Bongo hata hivyo hana kesi na aliachiliwa huru kutoka kifungo cha nyumbani lakini amesalia huko huko nyumbani.

Uchunguzi unaendelea nchini Switzerland ambapo Sylvia Bongo anadaiwa kutakatisha fedha.

Share This Article