Mwanamke akamatwa baada ya kupora raia wa kigeni Mombasa

Marion Bosire
1 Min Read

Maafisa wa upelelezi huko Nyali, Mombasa, wamemkamata mwanamke ambaye alipanga mpenzi wake wa asili ya Uingereza aibiwe baada ya kumhadaa na kumpeleka kwenye nyumba yake.

Mshukiwa huyo kwa jina Samira Mumbi Kiarie, amekuwa akimvizia jamaa huyo kwa miezi kadhaa sasa mtandaoni akimahidi upendo wa milele.

Jamaa huyo alishawishika na kuamua kuzuru makazi ya mwanamke huyo ya kifahari huko Nyali, asijue kilichokuwa kimepangwa.

dakika chache tu baada ya kufika huko, mlango ulifunguliwa kwa fujo, jamaa wawili wakaingia mmoja akijisingizia kuwa mume wa Samira na mwingine akijisingizia kuwa afisa wa polisi.

Aliyejifanya kuwa mume wa Samira alilaumu jamaa kutoka Uingereza kwa kuharibu ndoa yake huku polisi feki akitishia kumtia mbaroni.

Wawili hao walimlazimisha raia huyo wa kigeni kuwatumia shilingi laki 8, kwa nambari tofauti tofauti walizompa kabla ya kumtoa kwenye nyumba hiyo na kutoweka.

Baada ya kupashwa habari, maafisa wa upelelezi walianzisha uchunguzi na wakaweza kumkamata Samira na mmoja wa washirika wake aliyetambuliwa kama Paul Webster Mangeni almaarufu Paulo.

Uchunguzi umebaini kwamba wawili hao wamekuwa wakihadaa raia wa kigeni kupitia mitandao ya kijamii ya kuunganisha wapenzi, wanawapeleka kwenye nyumba za kukodisha kabla ya kuwapora.

Polisi wanamsaka mshukiwa wa tatu.

Share This Article