Ruto apokea mapendekezo ya mageuzi ya AU kabla ya mkutano wa Luanda

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto ambaye ni bingwa wa Umoja wa Afrika (AU) wa mageuzi ya kitaasisi, jana Jumanne alipokea mapendekezo ya kina kuhusu ajenda inayoendelea ya mageuzi ya AU kutoka kwa jopo kuu la wataalamu mashuhuri.

Mkutano huo, uliojumuisha wanachama wa Jopo Kuu la Utawala, Amani na Usalama wa AU, mwakilishi mkuu wa masuala ya ufadhili wa umoja huo, pamoja na maafisa wa ngazi ya juu kutoka Tume ya Umoja wa Afrika, ulilenga maandalizi ya mkutano maalum wa mageuzi ya AU utakaofanyika Novemba 26 mjini Luanda, Angola.

Ripoti ya pamoja iliyowasilishwa kwa Rais Ruto ilibainisha masuala muhimu ya kipaumbele, ikiwemo kufufua mifumo ya amani na usalama, kuhakikisha ufadhili endelevu wa umoja huo, kuwezesha Mahakama ya Haki ya Afrika kuanza kazi na kurahisisha ajenda na michakato ya maamuzi ya bunge la AU.

Majadiliano yalisisitiza umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya Utawala wa Afrika (AGA) na ile ya Amani na Usalama wa Afrika ili kukabiliana ipasavyo na changamoto mpya za bara.

Miongoni mwa mapendekezo makuu ni pamoja na kuiweka upya Afrika katika muktadha wa mabadiliko ya kisiasa duniani, kufufua Uafrika na kuimarisha uwezo wa kifedha wa kujitegemea wa umoja huo.

Mkutano huo ulitoa wito wa kujitolea upya kwa nchi wanachama wa AU na wadau wote ili kuharakisha mchakato wa mageuzi ya taasisi, kuhakikisha kuwa Umoja wa Afrika unakuwa tayari kikamilifu kuendesha utekelezaji wa dira ya maendeleo ya muda mrefu ya bara, Ajenda 2063.

Share This Article