Mwanamuziki wa mtindo wa Amapiano nchini Tanzania, Chino Kidd, ameendelea kuonyesha dhamira yake ya kuinua vipaji vipya baada ya kumtambulisha rasmi msanii chipukizi Mama Amina kwenye kampuni yake mpya ya kusimamia wanamuziki iitwayo WanaMan Gang.
Chino Kidd aliandika ujumbe wenye nguvu wa kumkaribisha msanii huyo mpya kwenye familia ya muziki wa mitaani kwenye akaunti yake ya Instagram akisema, “Karibu WanaMan Gang hiki ndicho chama cha wana kutoka mitaani.”
Mama Amina, ambaye amekuwa akivutia mashabiki kupitia mitandao ya kijamii kwa sauti yake ya kipekee na miondoko ya aina yake, sasa amepatiwa jukwaa rasmi la kukuza talanta yake akitafuta ushawishi zaidi ndani ya Tanzania.
Kampuni hiyo ya WanaMan Gang inatarajiwa kukua zaidi ya kazi ya kawaida ya burudani, kwani Chino Kidd ameonyesha kuwa ni harakati ya kusukuma mbele vipaji vya mitaani na kuunganisha kizazi kipya cha muziki.
Chino Kidd ambaye jina lake halisi ni Isaya Michael Mtambo alianza kama mcheza densi mwaka 2019 ambapo alifanya kazi na wasanii kama Rich Mavoko na Marioo kabla ya kuingilia muziki mwaka 2022.
Kibao chake cha kwanza alichotoa mwaka huo ni “Sina Msosi” lakini wimbo “Zuma” nsio ulimpa umaarufu zaidi nchini Tanzania.